Kwa ufupi:
Tumbaku ni moja ya zao kuu la biashara nchini. Tumbaku huipa nchi pato la kigeni kwa kuuzwa sana nchi za nje. Takwimu zinaonyesha kuwa mauzo nje ya nchi yameongezekwa kwa asilimia 50% kwa mwaka ulioishia 2013 kwa sababu ya kuongezeka kwa mauzo ya mazao ya biashara na tumbaku ikiwemo (BOT, 2013). Tumbaku hutoa ajira kwa kaya zaidi ya 90,000 ambazo huajiriwa mashambani na viwandani. Kwa ujumla takwimu zinaonyesha kuwa sekta ya tumbaku inasaidia kukuza uchumi kwa kaya zapatazo 450,000, sawa na asilimia 1.14 ya watanzania wote (FAOSTAT, 2014). Zao hili hulimwa katika maeneo mbalimbali nchini. Maeneo yanayolimwa zaidi tumbaku ni ya wilaya za Tabora, Kagera, Kigoma, Shinyanga, Iringa, Mbeya, Singida, Rukwa, Urambo, Kahama, Chunya, Kasulu, Ushetu, Manyoni, Nzega,Namtumbo, Songea, Kaliua, Sikonge, Uyui na Serengeti. Zao hili hulimwa na wakulima wadogowadogo wenye maeneo kati ya ekari moja hadi tano.Kuna aina tatu za tumbaku zinazolimwa hapa nchini. Aina hizo ni tumbaku ya kukausha kwa moshi, tumbaku ya kukaushwa kwa mvuke na tumbaku ya kukaushwa kwa jua. Hapa nchini Tanzania tumbaku inayolimwa kwa wingi ni tumbaku ya kukaushwa kwa mvuke (Flue Cured Tobacco) na tumbaku inayokaushwa kwa moshi (Dark Fire Cured Tobacco). Tumbaku ya moshi ilianza kulimwa wilayani Songea katika mkoa wa Ruvuma mnamo mwaka 1930 wakati tumbaku ya mvuke ilianza kuzalishwa kibiashara mkoani Iringa mwaka 1940 na baadaye wilayani Urambo mnamo mwaka 1951 baada ya mradi wa karanga uliokuwa chini ya wakoloni wa Kiingereza kushindikana na tumbaku kuchaguliwa kuwa zao mbadala la biashara badala ya karanga.