Kwa ufupi:
Mpunga ni moja ya zao muhimu zaidi la chakula katika Afrika Mashariki. Nchini Tanzania
mpunga unashika nafasi ya pili baada ya mahindi. Zao hili la chakula na biashara hulimwa kwa
wingi katika mikoa ya Shinyanga, Mbeya, Morogoro, Kilimanjaro, Mwanza, Tanga, Pwani,
Dodoma, Mtwara na Lindi. Inakadiriwa kuwa asilimia 30-40 za mpunga hupotea baada ya
kuvuna kila mwaka. Upotevu huu hutokana na teknolojia duni zinazotumika wakati wa kuvuna,
kusafirisha, kukausha, kupura, kuhifadhi na kukoboa.
Mvua ni chanzo kikuu cha maji kwenye kilimo cha mpunga. Viwango vya mahitaji ya maji
katika kukua kwa mpunga hutofautiana miongoni mwa aina za mpunga. Ni kwa jinsi hii mpunga
hupandwa katika mazingira mbalimbali kutegemea na mahitaji yake ya maji.
Zipo aina tatu kuu za mazingira yanayolimwa mpunga kulingana na upatikanaji wa maji na hali
ya mwinuko wa nchi. Mazingira haya ni kilimo cha mpunga wa mabondeni kinachotegemea
mvua (72%), kilimo cha mpunga wa kwenye miinuko (20%) na kilimo cha mpunga cha
umwagiliaji (8%).
Kiasi cha mpunga kinachozalishwa nchini kimekuwa kikiongezeka mwaka hadi mwaka kutoka
tani 41,000 mwaka 1970 hadi tani 811,500 mwaka 1998. Ongezeko hili limetokana na
kuongezeka kwa eneo linalolimwa mpunga na kwa kiasi kutokana na kuongezeka kwa miradi
midogo ya umwagiliaji pamoja na matumizi ya tekinolojia bora za kilimo.
Maeneo yanayolima mpunga kwa wingi Tanzania: ni Morogoro maeneo ya bonde la
kilombero/Ifakara, Dakawa, Malolo; Mbeya: Kyela, Mbarali; Shinyanga: Kahama; Mwanza,
Bonde la Ruvu mkoani Pwani. Na maeneo mengine mengi