Kwa ufupi:
Jumuiya ya Afya ya Nchi Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika imeendelea na uhamasishaji na msaada wa kitaaamu katika nchi husika ikiwemo Tanzania. Hii ni mojawapo ya mpango mkakati maalum wa kupunguza utapiamlo katika nchi hizi. Jumuiya inahamasisha kubadilishana uzoefu, taratibu sahihi, kubainisha vipaumbele, kujenga uwezo na kuhamasisha uwepo wa sera na program wezeshi zinazoboresha lishe katika nchi husika.Mafunzo kwa watoa huduma za lishe ni muhimu katika utekelezaji wa afua muhimu na zenye matokeo mazuri katika kuboresha lishe. Kuwajengea uwezo watoa huduma hao kutaongeza nguvu katika kuboresha wa utoaji wa huduma kwa walengwa katika ngazi zote. Aidha, Jumuiya ya Afya ya Nchi Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika uliandaa kitini cha mafunzo ya lishe kinacholenga kujengea uwezo, ujuzi na umahiri wezeshi kwa watoa huduma za lishe katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya na ngazi ya jamii. Maandalizi ya kitini cha mafunzo ya lishe yalitokana na matokeo ya tathmini katika uwezo wa kutoa huduma za lishe kwa kada mbalimbali iliyofanyika mwaka 2011 katika nchi za Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika uliofanywa na shirika la Hellen Keller International.Jumuiya imetoa rai kwa nchi zote kufanya mapitio na kurasimisha kitini hicho katika manzigira ya nchi husika ili watoa huduma za lishe waweze kutoa huduma stahiki. Tanzania pia ina upungufu wa wataalamu wenye elimu, ujuzi na umahiri wa kutosha kukidhi mahitaji ya utoaji wa huduma za lishe kwa jamii. Hivyo, serikali ya Tanzania, kupitia Wizara ya Afya Mandeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imefanya mapitio na kurasimisha kitini hicho ili kiweze kutumika kufundisha walengwa watakaotoa huduma na hatimaye kupunguza utapiamlo nchini.Kitini kimegawanyika katika makundi mawili, mojawapo ni kile cha Mafunzo ya Lishe kwa watoa huduma za afya katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma za afya. Kingine ni kile cha Mafunzo ya Lishe kwa Watoa Huduma za Afya Katika Ngazi ya Jamii. Ni matumaini yetu kwamba matumizi ya vitini hivi yataimarisha na kuongeza kasi na msukumo mpya wa taratibu mbalimbali zinazolenga kuboresha lishe nchini