Kwa ufupi:
Ulimwengu mzima una takribani watoto milioni 250 wenye umri chini ya miaka mitano ambao wanapatikana kwenye nchi zenye uchumi wa chini na zile zenye uchumi wa kati ambao wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua zao za ukuaji. Takribani robo tatu sawa na asilimia 66 ya watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano walio kusini mwa jangwa la Sahara wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji kutokana na kukosa malezi bora, umasikini, utapiamlo pamoja na matatizo mengine ya kijamii na kiuchumi. Hadi sasa maendeleo ya mtoto hayajapewa uzito unaostahili, badala yake msisitizo umewekwa kwenye kupunguza vifo licha ya kwamba kipindi cha miaka 0-8 ni fursa muhimu ya kuboresha maendeleo ya binadamu na hivyo kupata mtaji bora wa rasilimali watu yenye tija. Pia ifahamike kwamba, kukosekana kwa fursa za ukuaji kwa watoto wenye umri huo kunaweza kusababisha changamoto katika maendeleo yao ambayo yanaweza kuathiri kizazi na kizazi. Kumekua na hatua na jitihada mbalimbali katika kutatua changamoto za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM). Mifumo na miongozo mbalimbali imeandaliwa ikiwa imelenga kusaidia utekelezaji wa kina wa shughuli za MMMAM ili kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu. Miongoni mwa miongozo iliyoandaliwa ni ule wa malezi jumuishi uliozinduliwa na Shirika la Afya Duniani mwaka 2018 ambao una maono kuwa na “Dunia ambayo mtoto anaweza kufikia hatua zake za ukuaji na hakuna mtoto atakaeachwa nyuma” Mfumo huu wa malezi jumuishi unatoa mwongozo sahihi kwa nchi mbalimbali kuwekeza kwenye hatua zote za ukuaji wa mtoto.Tanzania ni moja ya nchi zenye uchumi wa kati wa chini ambapo asilimia 43 ya watoto wapo kwenye hatari ya kutokufikia hatua timilifu za ukuaji na maendeleo kutokana na viashiria vya hatari mbalimbali vya maendeleo kama vile utapiamlo, umasikini, kukosekana kwa uhakika wa chakula, msongo wa kifamilia, miundombinu duni na uhaba wa rasilimali pamoja na utelekezaji na unyanyasaji wa watoto. Vilevile wazazi au walezi kutokuwa karibu na watoto wao suala ambalo linachangiwa na kukosekana kwa uelewa wa kina wa MMMAM.Programu za malezi jumuishi nchini Tanzania zinahitaji kupewa kipaumbele na msisitizo kutokana na kukosekana kwa uratibu mzuri na zinatekelezwa kama sehemu za programu za kisekta au tafiti zinazofanywa na wadau zikilenga baadhi ya umri wa watoto na kutekelezwa kwenye maeneo machache.Kutokana na umuhimu wa Mfumo wa Malezi Jumuishi, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa MMMAM imeandaa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto itakayo tekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano (2021/22-2025/26). Mpango huu umelenga kutatua changamoto za ukuaji na maendeleo ya watoto wenye umri wa miaka 0-8. Programu hii itatoa mchango katika kufanikisha Mpango wa tatu wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano 2021/22 - 2025/26 kwa kutambua kwamba watoto ambao wanakosa kufikia kikamilifu hatua za ukuaji ni changamoto kwa maendeleo ya taifa na tishio kwa malengo ya kiuchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kujenga nchi ili kufikia uchumi wa kati. Kutokana na sababu hizo, programu hii imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya watu ili kuharakisha upatikanaji wa matokeo chanya ya maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali katika kutoa huduma za malezi jumuishi yenye vipengele vitano: afya bora kwa mtoto na mama/mlezi; lishe ya kutosha kuanzia ujauzito; malezi yenye mwitikio; fursa za ujifunzaji wa awali; ulinzi na usalama kwa watoto. Programu Jumuishi ya Taifa ya MMMAM inatakiwa izingatiwe na afua zote za malezi zitekelezwe kwa ujumuishi kwa kuwa inalenga kuleta matokeo chanya katika ukuaji na maendeleo ya awali ya mtoto na kufikia maono: “Watoto wote Tanzania wapo kwenye mwelekeo sahihi wa kufikia ukuaji timilifu”. Juhudi za wadau wote wa MMMAM na rasilimali zielekezwe kutekeleza afua zilizopangwa katika programu hii kwa wakati na ufanisi wa hali ya juu ili kufikia malengo ya programu. Wito unatolewa kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kusaidia kufanikisha maono ya programu hii kwa kuhakikisha wanajielekeza kuchangia utekelezaji kwa kufanya kazi kwa karibu na serikali. Aidha, upatikanaji wa rasilimali za kutosha (rasilimali fedha na watu) ni suala la muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa programu hii.