Kwa ufupi:
akwimu zinaonyesha kuwa eneo la misitu ya asili hapa Tanzania ni hekta (ha) 48,000,000 na misitu ya kupandwa ni ha 553,000. Inakadiriwa kuwa
uharibifu wa misitu ya asili ni ha 403,000 kwa mwaka. Uharibifu huu mkubwa
unasababishwa na mambo mengi hasa ongezeko la watu ambao shughuli zao
zinasababisha kilimo cha kuhama hama, idadi ya mifugo iliyozidi uwezo wa
eneo, uchomaji moto kiholela, upanuzi wa makazi na ukataji wa miti kwa
ajili ya matumizi mbalimbali. Athari za shughuli hizo ni pamoja na kukauka
kwa vyanzo vya maji, uhaba wa mazao yatokanayo na miti, uharibifu wa
mazingira na upoteaji wa bioanuwai.
Ili kukabiliana na uharibifu huu, njia mojawapo ni kuongeza kasi ya upandaji
miti na kudhibiti matumizi yake. Hili ni jukumu la kitaifa ambalo kila
mwananchi anapaswa kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wake.
Kabla ya kampeni ya kitaifa ya kupanda miti vijijini (Village Afforestation
Programme) kuanza rasmi mwaka 1970, kwa kiasi kikubwa jukumu la kupanda
miti na kusimamia misitu lilikuwa la serikali kupitia Idara ya Misitu na Nyuki.
Wakati wa kampeni hiyo, wananchi na taasisi mbalimbali zilihusishwa na
kuhimizwa kushiriki katika upandaji miti kwa ajili ya matumizi mbalimbali
chini ya dhana ya “Misitu ya Jamii” (Community Forestry).
Kutokana na Sera ya Taifa ya Misitu ya mwaka 1998, Sera ya Taifa ya Hifadhi
za Mazingira ya mwaka 2004 na Programu mbalimbali za kuhamasisha
upandaji miti kila mwaka, ni dhahiri kuwa Serikali inahimiza wananchi
na taasisi zishiriki kikamilifu katika suala la kupanda miti. Upandaji miti
unaweza kufanywa na taasisi za serikali, makampuni ya wawekezaji, vikundi
vya jamii, shule na hata watu binafsi. Miti inaweza ikapandwa peke yake
ikawa msitu, mti mmoja mmoja katika shamba, kuzunguka shamba, katika
maeneo ya makazi, kando kando ya barabara na penginepo kwa kuzingatia
ushauri wa wataalamu.
Kwa kuzingatia umuhimu wa kupanda miti na kuitunza, mwaka 1999
Wizara ya Maliasili na Utalii, kwa kupitia Mradi wa Taifa wa Mbegu za Miti
(National Tree Seed Programme - NTSP) sasa Wakala wa Mbegu za Miti
(Tanzania Tree Seed Agency - TTSA) ilichapisha kitabu kiitwacho “Aina ya
miti inayofaa kwa maeneo mbali mbali ya Tanzania Bara na maandalizi ya
bustani ya miche”. Kitabu hicho kilitokana na mada iliyotolewa na Dkt. Heriel
Msanga katika semina ya Wakuu wa Mikoa iliyofanyika huko Dodoma tarehe
15, Aprili 1999