Kwa ufupi:
Mwongozo huu unatoa maelezo juu ya teknolojia za kufuata ili kuwezesha
wakulima kufanya maamuzi kabla ya kuzalisha viazi mviringo,hasa katika
matumizi ya mbegu bora, mbolea, viuatilifu na mbinu bora za usimamizi wa
kilimo na mazingira. Nchini Tanzania viazi mviringo ni zao muhimu kwa chakula
na biashara. Kwa uzalishaji, viazi mviringo ni zao la tatu baada ya mahindi na
mpunga. Zao hili ni muhimu kwa usalama wa chakula, kuboresha lishe, ajira na
kuongeza kipato. Nchini Tanzania matumizi ya viazi mviringo yanaongezeka kwa
kasi vijijini na mijini kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu na mahitaji ya
vyakula vitokanavyo na viazi mviringo. Soko lake la uhakika ni kwenye miji mikuu
kama Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma. Masoko ya nje pia
yameendelea kuongezeka.
Kwa nyanda za juu kusini na kaskazini mwa Tanzania, mavuno ya viazi mviringo
ni makubwa ukilinganisha na mazao mengine ya chakula kama mahindi. Viazi
mviringo hukua vizuri katika miinuko ya kuanzia mita 1200 mpaka zaidi ya mita
3000 kutoka usawa wa bahari. Mikoa ya Mbeya, Iringa na Njombe inatoa zaidi ya
asilimia 80% ya viazi mviringo vinavyoliwa nchini Tanzania na ndio
inaongoza kwa uzalishaji wa viazi mviringo kwenye Nyanda za Juu kusini.
Viazi mviringo vinaweza kulimwa mara 3 kwa mwaka kila baada ya miezi 3-4
ukilinganisha na zao la mahindi linalochukua miezi 10-12 kwa baadhi ya
maeneo.